Meneja wa Benki ya Exim Tawi la Morogoro, Bi Anna Wesiwasi (wapili kulia) akipeana mkono na Mkurugenzi wa Kituo cha Amani cha watoto wenye ulemavu, Padri Beatus Sewando (watatu kulia) mara tu baada ya kuzindua jengo la kituo hicho kilichokarabatiwa na benki hiyo jana mkoani Morogoro. Akishuhudia ni Afisa Mauzo wa Benki hiyo Vick Haji (Kulia). Picha na mpiga picha wetu.
BENKI ya Exim Tanzania imefanya ukarabati wa majengo ya kituo cha watoto wenye ulemavu cha Amani kilichopo eneo la Chamwino mkoani Morogoro ikiwa ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo kuboresha maisha ya jamii.
Kupitia sera yake ya kurudisha sehemu ya faida yake kwa jamii, benki hiyo pia imejipanga kutoa misaada zaidi ikilenga mipango yenye kuleta maendeleo kwa jamii hapa nchini hususani katika maeneo ambayo benki hiyo tayari imefungua matawi yake.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya ukarabati wa majengo ya kituo hicho iliyofanyika mkoani humo mwishoni mwa wiki iliyopita, Meneja wa tawi la benki hiyo mkoani Morogoro, Bi Anna Wesiwasi alisema msaada huo pia unalenga uboreshaji wa maisha ya watoto wanaoishi kwenye kituo hicho kwa kuwa wataishi kwenye makazi salama, safi na bora kwa afya zao.
“Benki ya Exim siku zote tunaamini kuwa watoto wenye ulemavu wanahitaji kupewa matumaini zaidi na kwa kushiriki kwetu kwenye mipango ya maendeleo kama huu ndio tunatekeleza hiyo imani yetu kwa vitendo na zaidi tunazidi kuwa karibu na jamii inayotuzunguka jambo ambalo ni muhimu katika ulimwengu wa kibiashara kwa sasa kuona kwamba benki inarudisha sehemu ya faida yake kwa watu inao wahudumia,'' alisema Bi Wesiwasi
Kwa mujibu wa Bi Wesiwasi, benki hiyo inaamini kuwa watoto ndio wateja wao wa kesho kama sio wa sasa na hivyo basi benki hiyo itajitoa kwa hali na mali kuhakikisha kwamba wanapata maisha bora kwa sasa .
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Mkurugenzi wa kituo hicho, Padri Beatus Sewando alisema uamuzi wa benki hiyo kusaidia kituo cha watoto wenye ulemavu ni kitendo kinachotakiwa kuigwa na taasisisi, mashirika na watu mbalimbali hapa nchini.
“Tunashukuru sana kuona wenzetu wa benki ya Exim wameonyesha mfano kwa kuitikia kilio chetu.Msaada huu utawahakikishia watoto wetu hapa kituoni kuwa na makazi bora na salama kwaa afya zao…naomba wengione waige mfano huu,’’ alitoa wito
0 comments:
Post a Comment